Wakati Fulani nilihudhuria mafunzo ya
ujasiriamali yapata miaka 10 iliyopita. Mtoa mada alitaka kujua endapo kila
mshiriki angepewa milioni mia moja angefanya nini. Katika majibu
yaliyonishngaza ni pale mshiriki mmoja aliposema yeye angejenga hoteli eti kwa
sababu tuu baba mkwe wake alimwambia kuwa hoteli zinalipa.
Haikunishangaza mtoa mada alipotaka kujua
sababu ya kijana Yule kumwamini baba mkwe wake kiasi kile. Maya zaidi ni pale
alipoulizwa kama baba mkwe wake ana hoteli au aliwahi kumiliki hoteli, kijana
huyo alisema hapana.
Ni kawaida ya wajasiriamali wengi kufanya
vitu kwa sababu tuu wengine wanafanya bila kujali namna ya kufanya kitofauti
ili kuvutia wateja zaidi. Katika shughuli zangu za ushauri wa biashara nimewahi
kukutana na mama mmoja aliyekuwa anatubu na kujuta baada ya kushindwa kurudisha
mkopo aliochukua ili kuboresha biashara yake ya kupika na kuuza vyakula
almaanufu mama lishe/ntilie, alisema
“…….tulianza
kama wamama watatu hivi. Hakika wateja
walikuwa wengi na tulidhani kuna haja ya kuongeza mtaji ndipo nikakopa. Katika kipindi
cha miezi sita tuu tayari kulishakuwa na wakina mama wengine zaidi ya kumi
waliojiunga na kuanza kufanya biashara ya kuuza chakula. Kiukweli ilikuwa ni
kama tumewafumbua macho na kuwaonesha fursa ambayo walikuwa hawajaifahamu bado.
Cha kushangaza nikwamba kati yetu wote hakuna aliyekuwa akitoa huduma ya
tofauti na wenzake. Yani ni wali nyama ule ule na bakuli ya maharage/mchicha pembeni.
Taratibu tukaanza kuwekeana vinyongo kwa ajili ya kugombania wateja. Sasa hivi
ninavizungumza na wewe mama (jina limehifadhiwa) anamtuhumu mama (jina
limehifadhiwa) kwa kumloga ili biashara yake isifanikiwe…”
Hii ni sehemu ndogo tuu ya mifano
ninayokutana nayo kila siku ninapozungumza na wajasiriamali. Yamkini wajasiriamali
tungefahamu ni kwa namna gani ubunifu na huduma bora kwa wateja unavoweza
kuleta tija na ufanisi katika biashara. Tunapaswa kuamka na kuachana na fikra
za kizamani katika uanzishwaji na uendeshaji wa biashara zetu.
Nani kasema kuwa eti kwa sababu baba mkwe au
mtu Fulani kasema bishara ya hoteli inalipa basi uanzishe biashara ya hoteli. Je
unajua wateja wa hoteli wanataka nini? Je unajua kuna kundi gani la wateja wa
hoteli waliosahaulika na mfumo wa hoteli zilizopo. Labda wapo ambao shida yao
ni kulala tuu – nani kakwambia lazima uwawekee self contained yako na mi
breakfast yako inayofanya gharama kuwa maradufu?
Pengine wapo wanaotaka kuja kipumzika na
familia nzima – nani kakwambia uwajengee jihoteli lako lenyevyumba
vilivyopangana kama vya mabweni ya vyuo vikuu? Amka fikiria, kuwa mbunifu fursa
bado zipo achana na mawazo ya kizamani ya kuiga kila kitu?
Kwa wale walio mazingira kama ya Yule mama
lishe aliyenitembelea ofisini kwangu: Nani kakwambia kila mtu anapenda miwali
yenu ya nyama na maharage mliyokaanga kwa maguta yenye cholesterol isiyo na
kipimo? Nani kawaambia kila mtu anapenda kuja na kula anachokikuta?
Yawezekana wapo wanaopenda vyakula vya asili
vilivyochemshwa bila mafuta ( wazungu wanaviita natural foods). Kunaweza kukawa
pia na wale ambao wanaopenda kupikiwa kwa mahitaji maalumu. Amkeni kuweni
wabunifu, wateja hawaletwi kwa kulogana.
Mama lishe niliyemshauri leo ananishukuru
sana. Tunavozungumza yeye kaachana na miwali yenu ya mafuta na kukaanga. Hivi
sasa anauza ugali wa mtama, ndizi mchemsho, udaga samaki wa kuchemsha..nk. Hata
wenzake wamejaribu kumuiga lakini wameshindwa. Kwa kifupi amegundua kukaa kwake
kijijini kumsaidia kujua kupika vyakula vya kiasili kwa ladha ya kipekee
isiyowezwa kuigwa na mtu yoyote.
Yule kijana alifanikiwa kupata mkopo ingawa sikumbuki
ni shilingi ngapi. Ninachojua ni kwamba hoteli yake ipo katika orodha ya hoteli
zinazotarajiwa kupigwa mnada. Namwombea mugu ajitabue na kubadilika. Maana mpaka
sasa nahisi hajaelewa somo. Yeye anachojua ni kuilamu tuu serekaliu eti
imesababisha biashara yake kuwa ngumu. Mh! kwa kweli safari yake bado ndefu.
Hapo ni kuhusu ubunifu tuu kwa leo sitaki
hata kuzungumzia makosa tunyofanya katika kuwahudumia wateja. Siku nyingine
nitakuja na rafiki yangu Dotto Bulendu anisaidie kuwaeleza wakati tulipokuwa
safarini akamuuliza muhudumu wa ndege kama kuna kahawa au tangawizi alijibiwa
nini…
Nawatakia siku njema.
0 comments:
Post a Comment