Nilipokuwa safarini rafiki
yangu Dotto Bulendu alimuuliza muhudumu kama kuna uwezekano wa kupata kahawa au
tangawizi. Huku akiwa amekuja sura (labda kwa kukerwa na swali la bwana
bulendu) muhudum alijibu “….kwani wewe unataka nini?..”
Jibu alilopewa bwana doto na
mhudumu lilinisikitisha sana. Nilizidi kusononeka sana pale nilipoanza
kuitafakari taaluma na ueledi wa usimamizi wa biashara; mathalani nilizidi
kutatizwa na na nadharia ya huduma kwa wateja.Tofauti na wengi tunavodhani, taaluma ya biashara inasisitiza sana kuhusu nadharia za huduma bora kwa wateja hasa pale linapokuja swala la bishara za kuuza huduma kama vile: usafiri, tiba, mawasiliano na kadhalika
Mara nyingi wajasiriamali
tumekuwa tukiisahau nguzo hii muhimu ya huduma kwa wateja. Aghalabu utamkuta
mtu anakopa hela benki halafu anafanya kila kitu kinachohitajika katika misingi
ya biashara isipokuwa tuu rasilimali watu – binadamu anayeajiriwa kwaajili ya
kufanya kazi katika biashara ili kutimiza maono ya mwenye biashara.
Katika hali ya kawaida biashara
huanza na maono. Ndipo hapo tunaposema malengo na matarajio ya biashara
anayajua muanzilishi wa biashara yenyewe. Taaluma ya ujasirimali inashuhudia
kwamba bishara mpya itakuwa na uwezekano mkubwa wa kufanikiwa endapo tuu
waajiriwa (rasilimali watu) watakuwa wameelewa na kuiamini falsafa ya
aliyeanzisha biashara hiyo.
Changamoto kubwa ni kuwa na
rasilimali watu ambayo ipo kwa sababu ya uwepo tuu bila kuwa na uelewa wowote
kuhusu malengo na umuhimu wa kuifanya biashara husika kuwa endelevu kwa manufaa
ya vizazi vijavyo.
Laiti yule muhudumu angejua madhara
ambayo yangeweza kutokana majibu aliyomjibu bwana Dotto. Kwa mfano; kwa kupitia
tuu marafiki wa Doto, jamii inaweza kuwa na mtazamo hasi kuhusu kampuni husika.
Laiti mwenye kampuni hiyo ya usafiri angejua kuwa maono yake ya kutoa huduma
bora na kukikisha kuwa wateja wanaridhika na huduma bora inakwamishwa na
mhudumu aliyemuajiri.Ipo haja wajasiriamali kuwa makini na watu tunaowaajiri. Kuna njia nyingi za kuhakikisha kuwa wafanyakazi katika biashara yako wanatembelea falsafa iliyojikita katika maono yako. Semina za mara kwa mara juu ya falsafa ya kampuni ni muhimu. Pia vikao vifupi vya siku kabla na baada ya kazi ni muhimu kwani vinatoa mwanya wa kukosoana na kutambua zaidi uwezo wa watu uliowapa dhamana ya kufanya kazi katika biashara yako.
Mimi na dotto tumemsamehe yule
muhudumu lakini tumejiapiza kuwa hatutatumia tena huduma zake. Tumejiapiza kuwa
tutajitahidi kusisitiza huduma bora kwa wateja katika maeneo yetu ya kazi. Tumejiandaa
kwa changamoto hasa kutoka kwa wafanyakazi wenzetu ambao bado wanaamini kwenye
msemo wa chema chajiuza kibaya cha jitemebeza kwa asilimia mia moja.
Sisi tunasema sawa chema chajiuza
na kibaya chajiuza ila sio kwa asilimia mia moja. Tunaamini kuwa inawezekana
msemo huu ukawa sahihi kwingine. Ila linapokuja swala la huduma kwa wateja ni
kwa asilimia kadhaa; cha muhimu ni kutambua kuwa mteja ni mfalme na hakuna
biashara/mjasiriamali pasipo mteja.
Amka basi mjasiriamali
mwenzangu. Kuwa makini na chaguo katika rasilimali watu katika biashara yako. Usichoke
kuwaambia waajiriwa wako kuhusu umuhimu wa kuzingatia falsafa na maono yako. Nakutakia
mafanikio katika hilo. Siku nyingine nitakutembelea tujadiliane kuhusu fursa
zilizopo na changamoto katika chakula na kilimo. Nitaomba unisaidie kumuuliza
rafiki yangu kwa nini ameshindwa kutumia kalamu yake ya uandishi wa habari
kuielimisha jamii kuhusu fursa zilizopo katika kilimo.
0 comments:
Post a Comment