Mwaka 2008 mwandishi Giles
Boltoni alichapisha kitabu kilichoitwa “Aids and Othe Dirty Business” – Misaada na
biashara nyingine chafu. Hakika
kitabu hiki kina ufunuo mkubwa sana hasa kipindi hiki tunapoamua kusahau
mijadala ya msingi na kuwekeza nguvu nyingi kwenye kujadili deni la taifa.
Kwa kutumia uzoefu wake wa
kufanya kazi na mashirika ya misaada ya kimataifa, mwandishi Gill Bolton
anathibitisha kuwa mara nyingi misaada hailengi na haiwezi kuleta mapinduzi ya
kiuchumi katika nchi za zinazoendelea. Anahoji uhalali wa kuzipa nchi za kigeni
misaada huku gharama kubwa zikitumika kutekeleza malengo ya misaada hiyo (inaaminika
kuwa takribani asilimia 40 ya misaada hutumika tuu katika utawala wa miradi –
ambapo watawala wengi hutoka katikanchi wahisani huku wakilipwa mishahara
mikubwa kupindukia).
Ni maandiko ya kitabu hiki
yananifanya nielewe kwa nini tunaendelea kuwa masikini licha ya kuwa na
mashirika lukuki yenye kudai kuwa na malengo ya kuondoa umasikini. Haishangazi kukuta
taasisi yenye malengo ya kuondo umasikini vijijini lakini ofisi zake zipo Dar
es Salaam.
Ni kwanini misaada au mikopo
kutoka kwa wahisani haifikii malengo? Yamkini hili ni swali ambalo tulipaswa
kujiuliza kwanza. Mara nyingi misaada au mikopo huja na masharti ambayo hufanya
mikopo au misaada isiwe na ufanisi.
Kwa mfano umoja wa ulaya
unaweza kutupa mkopo au msaada masharti ya kuridhia mkataba wa bishara huria
kati Tanzania na nchi za ulaya. Kwa haraka harakaharaka ni rahisi kuhitimisha
kuwa Tanzania inaenda kunufaika kwani itapata wigo mkubwa kwa soko la bidhaa
zake.
Hii inaweza kuwa sahihi endapo
tuu mazingira wezeshi yatakuwepo. Kwa kutambua hilo mara nyingi wahisani huweka
vigezo kama ubora wa bidhaa, na uhuru katika uzalishaji – yaani watakwambia
serekali inapaswa kuiachia sekta binafsi bila kuiingilia. Mara nyingi mwanya wa
soko huria hutumika na wahisani kuzuia jitihada zozote za serekali katika
kuisaidia sekta binafsi kuwa katika uwezo kutoa bidhaa zinazoweza kushindana
katika soko la kimataifa.
Kwa maana hiyo basi Gill Bolton
anatuonesha kuwa ni vigumu misaada na mikopo kufikia malengo kwani hata watoa
misaada/mikopo wenyewe hawana nia ya kusaidia wakopaji zaidi ya kuwafunga
kitanzi. Kwenye kitabu “Confession of an
economic hitman” John Perkins anaeleza jinsi mikopo inavyorudi kwa
wakopeshaji kwa kutumia makampuni yanayotoka nchi za wakopeshaji yanapopewa
kandarasi za kutekeleza malengo ya mikopo. Anasema “ mwisho inakuwa ni nchi
zilizoendelea kuzinyonya nchi zinazoendelea kwa kupitia kigezo cha mikopo na
misaada.
Kwa kuwa imepita takribani
miongo sita tangu tupate uhuru; na kwakuwa katika kipindi chote hiki mikopo na
misaada kutoka wahisani haijaweza kupunguza umasikini kwa kiasi kikubwa;
tunapaswa kubadili mtazamo na kurudi nyuma na kujipanga na mbinu mpya za
kuondoa umasikini.
Tunapaswa kukopa mikopo ambayo
inatupa uhuru wa kuwekeza katika Nyanja tunazoamini kuwa zitatuletea tija. Mathalani
uwekezaji kwenye miundominu kama reli, barabara, viwanja vya ndege na
kadhalika; na uboreshwaji wa mifumo ya uwekezaji kwenye kilimo unapaswa kuungwa
mkono.
Ni kwa kupitia jitihada zetu
pekee tutaweza kupambana na umasikini. Haitatokea mtu aje kutupa msaada eti kwa
kuwa anapenda tusiwe masikini. Tuelewe pia vita ya umasikini ni kubwa na ngumu.
Tujifunze kutoka maanguko ya Torijos (Panama), Muamar Ghadaf (Libya), Patrice
Lumumba (Zaire), Hugo Chavez (Venezuela) na ambacho kinachotokea kwa Maduro (Venezuela)
na Babu Robert Mugabe (Zimbabwe). Wote hawa kwa namna moja au nyinginewamekuwa
wahanga wa juhudi za kufanya mataifa yao kuwa na uhuru wa kiuchumi.
0 comments:
Post a Comment