Hot!

HABARI YA KUANZISHWA KWA FACEBOOK NA FUNDISHO KWA WAJASIRIAMALI JUU YA KUWA MBUNIFU NA KUULINDA UBUNIFU


Mwaka 2009 Ben Mezrich aliandika kitabu kilichoitwa, “Accidental Billionnaires: The founding of facebook, a tale of sex, money, genious and betrayal”. Kwa hakika kitabu hiki kinatoa fundisho kubwa sana kwa wajasiriamali wa kitanzania na duniani kwa ujumla.

Ukisoma kitabu hiki kilichosheheni utafiti yakinifu wa habari ya kuundwa kwa facebook – mtandao maarufu wa kijamii, utagundua umuhimu wa ubunifu na jinsi ya kuhakikisa kuwa ubunifu huo unalindwa na kuwa endelevu.

Pamoja na kwamba wazo la kuanzisha facebook lilianzia kwa mapacha wawili (maarufu kwa jina la Winklevos twins) na kuchagizwa na mtaji wa kwanza (capital seed) uliotolewa na Eduardo Saverin (rafiki aliyekuwa anaishi na mmiliki wa sasa wa facebook), ni Mark Zuckerberg pekee anaeonekana shujaa kwa sasa.

Ndio ubunifu ni mzuri lakini tunapaswa kuwa makini na tunaowashirikisha mawazo yanayotokana na ubunifu wetu. Mark Zukerberg alikuwa na utaalamu wa kuweza kuanzisha facebook lakini je asingekutana na hao mapacha angeweza kuwa na hilo wazo?

Katka moja ya majadiliano kati ya Zuckerberg na Winklevos twins, kunaibuka hoja ya facebook itakuwa na utofauti gani na mitandao mingine za kijamii (kwa wakati huo twiter na My Space). Kwa the winklevos twins jibu lilikuwa ni rahisi tu – hwrvard.edu. Waliamini kuwa na mtandao wa kijamii wenye domain ya Harvard kungewavutia wanachuo wengi kujiunga.

Tunkumbuke kuwa nilipowasimulia hadithi ya mama lishe tuliona umuhimu wa kuwa na kitu tofauti kwenye biashara. Kwa facebook ilikuwa hivyo hivyo. Mbali na kuwa na domain ya havard, kadiri siku zilivokuwa zinaenda Mark Zuckerberg na timu yake waliendeleza ubunifu na kuifanya facebook kuwa chaguo la wengi katika jamii. Taratibu thamani ya facebook ikapanda mpaka kufikia hatua ya Mark Zukerberg kuwa tajiri kijana zaidi duniani.

Mbali  na kuwa mbunifu changamoto kubwa huja katika kuhakikisha ubunifu unalindwa na kuwa endelevu. Taaluma ya biashara inaonesha kuwa zipo njia mbalimbali mbali za kutunza ubunifu. Njia hizo zinatofautiana kuendana na mazingira, malengo na wakati mwingine aina ya biashara.

Kwa mfano kama biashara inahusu uzalishaji wa chakula au kinywaji njia rahisi ni kujimilikisha kanuni (formular) kwa kuisajili kisheria na kuhakikisha haiigiki kirahisi – Coca Cola, watengenezaji wa pipi za ivory na kampuni zinazotoa huduma ya teknolojia wamefanikiwa sana kwa kutumia njia hii.

Endapo biashara inahusu kutoa huduma utunzaji wa ubunifu unaweza kuwa changamoto kwa kiasi fulani. Na wakati mwingine wajasiriamali/wamiliki wa biashara wanalazimika kuchanganya ubunifu na unafuu wa gharama. Biashara zinazofanikiwa kwenye Nyanja za usafiri, hoteli na utalii zimekuwa zikitumia sana kwa kutumia mbinu hii.

Wakati mwingine inapokuwa vigumu kushindana kwenye ubunifu au mchanganyiko wa uubunifu na upungufu wa bei, njia pekee inayobaki ni kumnunua mpinzani wako au mpinzani wa mpinzani wako. Mara nyingi matokeo ya njia hii ni kujimilikisha soko kwa kubaki mwenyewe sokoni au kupunguza idadi ya washindani ili kuongeza ufanisi.

Mfano mzuri ni tukio la miaka ya hivi karibuni la facebook kuinunua kampuni ya watsap ili kupunguza usindani. Yote kwa kwa yote habari ya facebook inatupa fundisho la historia nzima ya jinsi mjasiriamali wa kawaida anavyoanza na ubunifu wake na changamoto anazoweza kuzipitia kabla ya kupata mafanikio.

Kwa Winklevos twins tunapata fundisho la kuwa makini na ubunifu wetu, kwani wapo waliozoea kutembelea nyota za watu kwa kuiba mawazo ya watu wengine na kuyafanya ya kwao katika biashara. Laiti kama wangeingia mkataba wa kisheria  na Zuckerberg kwa kumuajiri kama mtaamu wa kompyuta leo hii face book ingekuwa ya kwao.

Kwa Zuckerberg tunapata fundisho la kuhakikisha ubunifu ni endelevu. Kwa kuinunua watsap facebook itabaki kuwa moja ya mitandao bora ya kijamii kwa muda mrefu. Ewe mbunifu mwenzangu umeshafikiria namna ya kutunza ubunifu wako? Au unangoja mpaka uanguke kama mimi halafu ubaki kuilamu serekali yako?

Mimi nilianguka nikaamka. Naamini sitaanguka tena maana nimejifunza mengi kwenye kuanguka kwangu. Winklevos twins na Eduardo Saverin waliangushwa na Zuckerberg. Sina uhakika kama walishaamka au la? Ila nina uhakika anguko lao ni fundisho kwa wengi.

Amka mjasiriamali mwenzangu kuwa mbunifu. Hata mdogo wangu Humphrey Mgonja kaamua kuwekeza kwenye ubunifu katika tasnia ya uandishi wa habari; na ndio maana kaiona fursa kwenye kanisa la viziwi na habari ya mbuzi wanaoishi mjini kama binadamu. Fursa ambazo waandishi wenzake hawakuziona hapo mwanzo

Kwa heri kwa leo ila nakusisitiza tena ndugu yangu uamke ili miaka ya mbeleni Ben Mezrich apate kuandika kitabu juu jinsi ulivoamka kutoka kwenye anguko lako na kuwa mfanya biashara uliyefanikiwa zaidi Tanzania.

0 comments:

Post a Comment