Hot!

Pale Mwehu Anapogeuka Kuwa Mjasiriamali


 
Takribani miongo mitatu iliyopita muokota makopo alikuwa akionekana mwehu. Yani kulikuwa na msemo maarufu uliosema “ unaniita kichaa kwani naokota makopo” kwa wakati huo ilikuwa ni nadra kumkuta binadamu mwenye akili timamu akiokota makopo mitaani.
Ama kweli siku hazigandi. Nimelazimika kuamini dunia inabadilika. Ndio! Tanzania inabadilika na tunaweza kusema Daresalam inabadilika na itaendelea kubadilika. Eti leo muokota makopo anaitwa mjasiriamali.
Nimeshtushwa na kasi ya waokota makopo ambao kwa hali inavyoenda inaweza kufika mahali wakawa kero kwenye  nyumba za watu. Imekuwa kawaida kwa siku za hivi karibuni kusikia mtu akigonga geti. Eti anauliza kama kuna chupa za plastiki.

Ni hali hii inayonivutia na kunifanya niwaze kufanya utafiti juu ya biashara hii ya kuokota makopo. Naanza kujiuliza nini kimeongezeka kwenye chupa hizi za plastiki ambacho hakikuwepo miongo miwili iliyopita? Najiuliza tena ni nini kilichoongezeka katika makopo na vyuma chakavu vya sasa ambacho hakikuwepo miongo miwili iliyopita?
Katika kutafiti kwangu nagundua kuwa hakuna kilichobadilika katika chupa makopo au vyuma chakavu. Vyuma ni vile v ya miongo miwili iliyopita. Hali hii inanivutia kutaka kujua kutoka kwa anaefanya biashara ya kuuza vyupa vya plastiki au vyuma chakavu. Kwakuwa muda umeshaenda najipa moyo kwamba kesho lazima nitafute mtu  anaefanya niashara hii ili ipate undani.

Kama ilivyo ada kwa wengi naamua kwenda kuimalizia siku yangu katika ukumbi wa mazoezi ya viungo. Najisogeza kivivu huku nikitamani muda uende haraka – asikudanganye mtu , hakuna kazi ngumu kama kufanya mazoezi ya viungo.

Ninachokikuta kwenye ukumbi wa mazoezi kinarudisha fikra zaku masaa kadhaa nyuma.  Namuona kijana mmoja aliye makini sana. Mkononi kashika mfuko wa plastiki almaarufu mifuko ya Rambo. Ukimtazama kijana huyu anavoangalia watu kwa makini utadhani ni mlinzi wa ukumbi au askari magereza anaesimania wafungwa wakifanya kazi ngumu.
Umakini wote wa kijana huyu umelenga kwenye kuhakikisha anamuwahi kila anaekunywa maji ili amuachie chupa tupu baada ya kumaliza. Dah! Kumbe utafiti niliopanga kuufanya kesho ninaweza kuufanya leo.

Namdadisi kijana huyu muokota chupa za maji ili kujua kwa nini ameamua kufanya kazi iyo. “…..hii kazi inalipa sana braza. Kwa siku sikosi elfu 5 mpaka kumi. Kimsingi nimeamua kujiajiri na ninajivunia kwa kazi ninayofanya……” ananiambia.
Kumbe janga la uchafuzi wa mazingira lmegeuka kuwa fursa. Mwalimu wangu wa ujasiriamali aliwahi kuniambia kuwa,  biashara nyingi zilizofanikiwa ni zile zilizotokana na changamoto.

Hapo ndipo ninapokumbuka safari yangu ya nchi moja ya jirani pale niliposhudia kampuni inayokusanya kinyesi cha binadamu na kukigeuza kuwa mbolea na baadae kuwauzia watu. Nakumbushwa zaidi na habari ya kampuni ya kigana inauotumia taka ngumu kutengeneza mbolea asilia.
Hakika namaliza siku nikiwa nimehamasika. Najiapa moyo, najiambia kuwa ipo siku na mimi nitabadilisha changamoto kuwa fursa. Amka mjasiriamali mwenzangu. Amka tufikirie nje ya boksi ili tuvumbue ni changamoto gani tunazoweza kuzigeuza kuwa fursa.

Kwaheri kwa leo mjasiriamali mwenzangu ila nakuomba unapowaza juu ya kugeuza changamoto kuwa fursa ujiulize: yupo wapi Yule mtanzania aliyevuma kwenye vyombo vya habari kwa kutengeneza roboti kwa ajili ya kulinda usiku? Yupo wapi yule kijana aliyegundua teknolojia ya kuzima umeme kwa kutumia simu hata kama mtumiaji yupo kilomita elfu moja kutoka ilipo nyumba yake?
Sikutishii ndugu yangu, nakupa tuu changamoto ili uweze kufikiri nje ya boksi. Haya basi pumzika. Ingawa wakati unapumzika nakuasa ujiulize ni kwa nini mgunduzi wa power bank ya Puku (ambaye ni mtanzania)  kaisajili kampuni yake marekani badala ya Tanzania?

0 comments:

Post a Comment