Hot!

Other News

More news for your entertainment

KWA NINI TUNAPASWA KUKATAA MISAADA NA MIKOPO KUTOKA NCHI ZA KIGENI?


Mwaka 2008 mwandishi Giles Boltoni alichapisha kitabu kilichoitwa “Aids and Othe Dirty Business” – Misaada na biashara nyingine chafu. Hakika kitabu hiki kina ufunuo mkubwa sana hasa kipindi hiki tunapoamua kusahau mijadala ya msingi na kuwekeza nguvu nyingi kwenye kujadili deni la taifa.

Kwa kutumia uzoefu wake wa kufanya kazi na mashirika ya misaada ya kimataifa, mwandishi Gill Bolton anathibitisha kuwa mara nyingi misaada hailengi na haiwezi kuleta mapinduzi ya kiuchumi katika nchi za zinazoendelea. Anahoji uhalali wa kuzipa nchi za kigeni misaada huku gharama kubwa zikitumika kutekeleza malengo ya misaada hiyo (inaaminika kuwa takribani asilimia 40 ya misaada hutumika tuu katika utawala wa miradi – ambapo watawala wengi hutoka katikanchi wahisani huku wakilipwa mishahara mikubwa kupindukia).

Ni maandiko ya kitabu hiki yananifanya nielewe kwa nini tunaendelea kuwa masikini licha ya kuwa na mashirika lukuki yenye kudai kuwa na malengo ya kuondoa umasikini. Haishangazi kukuta taasisi yenye malengo ya kuondo umasikini vijijini lakini ofisi zake zipo Dar es Salaam.

Ni kwanini misaada au mikopo kutoka kwa wahisani haifikii malengo? Yamkini hili ni swali ambalo tulipaswa kujiuliza kwanza. Mara nyingi misaada au mikopo huja na masharti ambayo hufanya mikopo au misaada isiwe na ufanisi.

Kwa mfano umoja wa ulaya unaweza kutupa mkopo au msaada masharti ya kuridhia mkataba wa bishara huria kati Tanzania na nchi za ulaya. Kwa haraka harakaharaka ni rahisi kuhitimisha kuwa Tanzania inaenda kunufaika kwani itapata wigo mkubwa kwa soko la bidhaa zake.

Hii inaweza kuwa sahihi endapo tuu mazingira wezeshi yatakuwepo. Kwa kutambua hilo mara nyingi wahisani huweka vigezo kama ubora wa bidhaa, na uhuru katika uzalishaji – yaani watakwambia serekali inapaswa kuiachia sekta binafsi bila kuiingilia. Mara nyingi mwanya wa soko huria hutumika na wahisani kuzuia jitihada zozote za serekali katika kuisaidia sekta binafsi kuwa katika uwezo kutoa bidhaa zinazoweza kushindana katika soko la kimataifa.

Kwa maana hiyo basi Gill Bolton anatuonesha kuwa ni vigumu misaada na mikopo kufikia malengo kwani hata watoa misaada/mikopo wenyewe hawana nia ya kusaidia wakopaji zaidi ya kuwafunga kitanzi. Kwenye kitabu “Confession of an economic hitman” John Perkins anaeleza jinsi mikopo inavyorudi kwa wakopeshaji kwa kutumia makampuni yanayotoka nchi za wakopeshaji yanapopewa kandarasi za kutekeleza malengo ya mikopo. Anasema “ mwisho inakuwa ni nchi zilizoendelea kuzinyonya nchi zinazoendelea kwa kupitia kigezo cha mikopo na misaada.

Kwa kuwa imepita takribani miongo sita tangu tupate uhuru; na kwakuwa katika kipindi chote hiki mikopo na misaada kutoka wahisani haijaweza kupunguza umasikini kwa kiasi kikubwa; tunapaswa kubadili mtazamo na kurudi nyuma na kujipanga na mbinu mpya za kuondoa umasikini.

Tunapaswa kukopa mikopo ambayo inatupa uhuru wa kuwekeza katika Nyanja tunazoamini kuwa zitatuletea tija. Mathalani uwekezaji kwenye miundominu kama reli, barabara, viwanja vya ndege na kadhalika; na uboreshwaji wa mifumo ya uwekezaji kwenye kilimo unapaswa kuungwa mkono.

Ni kwa kupitia jitihada zetu pekee tutaweza kupambana na umasikini. Haitatokea mtu aje kutupa msaada eti kwa kuwa anapenda tusiwe masikini. Tuelewe pia vita ya umasikini ni kubwa na ngumu. Tujifunze kutoka maanguko ya Torijos (Panama), Muamar Ghadaf (Libya), Patrice Lumumba (Zaire), Hugo Chavez (Venezuela) na ambacho kinachotokea kwa Maduro (Venezuela) na Babu Robert Mugabe (Zimbabwe). Wote hawa kwa namna moja au nyinginewamekuwa wahanga wa juhudi za kufanya mataifa yao kuwa na uhuru wa kiuchumi.